Na Mwandishi Wetu, Mbeya.
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro ameipongeza Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kutokana na bia ya Safari Lager kutwaa Tuzo ya Bia Bora Afrika.
Kandoro alimwaga sifa hizo wakati akipokea kombe la ushindi huo ambalo lilioneshwa mahususi kwa wakazi wa Mbeya, katika sherehe zilizofanyika kwenye Viwanja vya Kabwe vilivyopo Mwanjelwa mjini hapa jana.
Alisema ni faraja kubwa kwa Watanzania kutokana na bia ya Safari Lager kutwaa tuzo hiyo na kufanikiwa kuzishinda bia zote barani Afrika kwa ubora.
“Tunashukuru tumeletewa kuliona kombe mlilolipata kutokana na ubora wa bia yenu, hii ni furaha kwa Watanzania na naamini ushindi huu utachochea watu kupenda bidhaa zao.
“Kufanikiwa kutwaa Tuzo ya Bia Bora Afrika si kitu kidogo, ni faraja kwetu sote na sasa tunaweza kujivunia kile kilicho chetu,” alisema Kandoro.
Sherehe hiyo ya kulionyesha kombe kwa wakazi wa Mbeya kuliambatana na burudani za kila aina, ambazo zilitolewa na vikundi kadhaa vya muziki.
Akizungumzia ushindi huo, Meneja wa bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo alisema ni wa kujivunia zaidi na wao watahakikisha wanaendelea kuzalisha bidhaa bora zaidi.
0 comments:
Post a Comment